Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMBI ya wazee wenye ulemavu wa ukoma iliyopo Msufini Kata ya Ngomeni wilayani
hapa, Mkoa wa Tanga inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa vitanda hali inayosababisha kulala chini.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi, wazee hao wameiomba Serikali na wadau wengine kuangalia namna ya kuwasaidia ili waondokane na adha inayowakabili kwa muda mrefu.
Joseph Mshigao, alisema alifika kambini hapo tangu mwaka 1984, ambako licha ya ulemavu alionao amekuwa akiamka asubuhi mwili wake ukiwa umechoka kutokana na kulala chini.
Mshigao, alisema kutokana na kulala chini pia hung’atwa na wadudu kama ng’e na nyoka, kwani nyumba zao zina nyufa zinazotokana na kutofanyiwa ukarabati mara kwa mara.
Mwenyekiti wa makazi ya wazee hao, Juma Bakari, alisema upo umuhimu kuwa na vitanda kituoni hapo ili kuwapunguzia adha wanayoipata, kwani wengi wao hawana baadhi ya viungo vya mwilini.
"Tunaiomba serikali na wadau wote watuangalie kwa jicho la huruma, kwani tunapata tabu kukosekana kwa vitanda hali inayopelekea kuishi kwa mashaka, wakati mwingine tunaona kuanzishwa kwa kambi hii kwetu kama vile ni mateso," alisema.
Kituo hicho kinachokadiriwa kuwa wazee 40, kilitengwa kwa ajili ya watu waliokuwa wakiugua ugonjwa wa ukoma ndani ya Mkoa wa Tanga.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment