Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Familia ya Jaji Lewis Makame imesema haitasahau namna jaji huyo
alivyoijali na kulitumikia taifa kwa uaminifu hadi mauti yalipomfika
juzi mchana.
Akizungumzia utaratibu wa maziko ya kiongozi huyo
jana, mwanaye Eugene alisema kutokana na mchango wake mkubwa kwa familia
na kwa taifa, watatumia siku nne ili kutoa fursa kwa familia na
viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kutoa heshima zao za mwisho.
Alisema kwa sasa familia inaendelea kuratibu na
kusimamia utaratibu wa awali wa maziko yake yanayotarajiwa kufanyika
katika Kijiji cha Tongwe Muheza, mkoani Tanga ambako alizaliwa.
“Hadi sasa tunaendelea na maandalizi ya maziko ya
mzee wetu na ibada maalumu ya kumuaga itafanyika hapa nyumbani siku ya
Ijumaa asubuhi kabla ya kuelekea Kanisa la St Alban na baadaye
tutampeleka katika Kijiji cha Tongwe kwa ajili ya kuupumzisha mwili wake
kwa amani,” alisema Eugene.
Alisema baba yake alifariki dunia juzi saa 7.45
mchana katika Hospitali ya AMI Trauma, Masaki, alikokuwa amelazwa kwa
takriban mwezi mmoja.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete amemtuma salamu
za rambirambi kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na
familia ya marehemu kutokana na kifo hicho.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Ikulu, ilisema Rais amepokea taarifa za kifo hicho kwa
masikitiko, kwa kuwa ni miongoni mwa watu waliolitumikia Taifa kwa
uaminifu, uadilifu, bidii na umahiri mkubwa.
Rais Kikwete alisema uongozi wake ulichangia
kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa katika
mazingira mapya ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
Chadema watoa salamu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nacho
kimetuma salamu za rambirambi na kusema kuna haja ya kupongeza utumishi
wake katika kipindi chote alichokuwa akilitumikia Taifa akiwa
mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment