Home » » MAMBEA ATAKA MASHAMBA YAGAWANYWE KWA WANANCHI

MAMBEA ATAKA MASHAMBA YAGAWANYWE KWA WANANCHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wametaka mashamba ya mkonge yaliyotelekezwa kwa muda mrefu yagawiwe kwa wananchi ili waweze kulima na kujenga makazi.
Hayo yalisemwa juzi kwenye maswali ya papo kwa hapo na Diwani wa Kata ya Marungu, Mohamed Mambea kwenye Baraza la Madiwani wa Jiji la Tanga na kusema kata yake inamashamba mawili ya mkonge yaliyotelekezwa, lakini sheria inawabana wananchi kuweza kuyatumia kwa kilimo.
"Kata ya nguya Marunguku na mashamba mawili ya mkonge ambayo yamekufa au kushindwa kuendelezwa zaidi ya miaka 20 sasa. Na sheria ya ardhi inasema, ardhi ikitelekezwa kwa zaidi ya miaka 12 mtu mwingine akiendeleza ardhi hiyo sheria inamtambua anayo haki.
"Katika maeneo hayo wananchi wa Kijiji cha Geza, Marungu na Mkembe wamejenga na kulima kwenye maeneo hayo. Je ni liniyatapelekwa kwa Rais ili kufuta hati na kuweza kupewa wananchi," alisema Mambea.
Mambea alisema pia kuna mradi wa maji unaogharamiwa na Benki ya Dunia kwenye vijiji vitano vya kata vya Marungu , Geza, Kirare, Mapojoni na Mwarongo, lakini mradi huo unasuasua na hawajui hatima yake .
Naye Diwani wa Kata ya Msambweni, Abdulraham Hassan Omar alisema Halmashauri ya Jiji imetoa ardhi yenye thamani ya sh.bilioni 3.5 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda eneo la Pongwe, lakini mradi huo ni kama umesimama, kwani hawaoni kitu kinachoendelea.
"Mradi huu umekuwa unasuasua kwa muda mrefu bila kuendelezwa. Halmashauri ina utaratibu gani kwa kuzingatia thamani ya ardhi inapanda siku hadi siku, na utaratibu gani unafanyika kwa kuzingatia muda na mikataba," alisema Omar.
Akijibu baadhi ya maswali hayo, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Omar Guledi alisema mashamba hayo kwa muda mrefu yalikuwa na kesi mahakamani, hivyo ili kuonekana hayaendelezwi ni lazima hesabu ya miaka ianze baada ya kumalizika kesi, hivyo bado hayajafikisha miaka ya kufutiwa hati zake.
"Kuhusu maji Serikali imesema haina fedha, ila kama mkandarasi ataendelea na ujenzi kwa fedha zake, basi Serikali itakuja kumrudishia," alisema Guledi.
Naye Mkurugenzi wa Jiji hilo Juliana Malange alisema ni kweli wameingia mkataba na Kampuni ya Good PM ya Korea kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo, lakini mchakato wake bado unaendelea kwani umehusisha watu wengi ikiwemo Mamlaka ya Uwekezaji Kanda Maalumu (EPZA) na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa