WANANCHI wa Kijiji cha Kwefingo kilichopo Kata ya Dindira, wilayani
Korogwe, walizuia msafara wa Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen
Ngonyani ‘Profesa Majimarefu’, ili waweze kumweleza kero zao.
Wananchi hao waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali,
walimsimamisha mbunge huyo baada ya kumaliza mkutano wa hadhara katika
kijiji hicho.
Akiwasilisha kero hiyo mbele ya mbunge huyo, Ismail Bendera, alisema
wanashangaa kuona nguzo za umeme zikiwekwa katika Kijiji jirani cha
Mgwashi badala ya umeme huo kuanza kufika katika kijiji chao ambacho
ndipo makao makuu ya kata hiyo.
“Tunashangaa tumewahi kukusikia bungeni ukitaja kwamba umeme utakuja
hapa katika kijiji chetu, lakini mbona sasa tunaouna umekwenda katika
kijiji ambacho anatoka diwani?” alihoji Bendera.
Mkazi mwingine, Bakari Kibwana, alisema wamesikia taarifa kwamba
umeme hautafika katika kijiji chao na kwamba endapo suala hilo litakuwa
kweli watakuwa tayari kufunga ofisi za kata ili kushinikiza umeme
ufike katika kijiji chao.
Akijibu maswali hayo, mbunge huyo alisema suala la umeme huo ambao ni
mpango wa serikali wa usambazaji wa umeme vijijini (REA), katika jimbo
lake utasambazwa katika vijiji kumi kijiji chao kikiwemo.
Aliwatajia vijiji hivyo kata zake zikiwa kwenye mabano kuwa ni
Kwefingo (Dindira), Mgobe na Gereza (Makuyuni), Mkwakwani na
Kwemzindawa (Mnyuzi), Lusanga na Makumba (Kerenge), Alamisi,
Matalawanda na Kijango (Magoma) na Kijiji cha Vugiri kilichopo Kata ya
Vugiri.
Hata hivyo aliwahakikishia umeme utafika katika kijiji hicho na
kwamba atafuatilia kujua namna watakavyoufikisha katika kijiji hicho.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment