Home » » Utoro Watishia Sekondari za Kata Korogwe

Utoro Watishia Sekondari za Kata Korogwe


Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlungui iliyopo Kata ya Bungu
wilayani Korogwe, Sylvester Msigwa akizungumza shuleni hapo.
Mwalimu wa Taaluma wa Sekondari ya Kwagunda, Halila Mohamed akizungumza na mwandishi wa Thehabari.com (hayupo pichani).
Baadhi ya wanafunzi Sekondari ya Kwagunda wakizungumzia changamoto mbalimbali za elimu.
Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya Kwagunda moja ya shule za kata wakizungumzia changamoto mbalimbali za elimu.
---


UTORO wa kudumu kwa idadi kubwa ya wanafunzi wa
Sekondari hasa zile za Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe unatishia
maendeleo ya elimu eneo hilo.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari
hizi juzi kwa baadhi ya sekondari umebaini hali hiyo sasa inatisha kwani
inaongezeka kwa kasi karibuni katika kila shule za sekondari eneo hilo.

Katika sekondari za Kwagunda, Kwashemshi,
Mulungui pamoja na Bungu vitendo vya utoro wa kudumu kwa wanafunzi vinaongezeka
kwa hali ya juu jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya elimu eneo hilo.

Akizungumzia hali ya utoro, Mwalimu wa Taaluma
wa Sekondari ya Kwagunda, Halila Mohamed alisema shule hiyo hupokea wanafunzi
180 wanaojiunga kidato cha kwanza kila mwaka lakini wanaofika kidato cha nne ni
80 pekee, huku idadi kubwa wakiishia kutoroka.

Alisema idadi kubwa ya watoro hukimbilia
kufanya vibarua katika machimbo ya matofari ya kuchoma kijijini hapo huku
wengine wakifanya vibarua kwa wakulima na wafugaji wanaozunguka eneo hilo.

“Kibaya zaidi hutoroka na baadhi yao kuonekana
kwenye mitihani tu...kimsingi mwamko wa elimu eneo hili bado upo chini sana kwa
wanafunzi wenyewe pamoja na wazazi wao...,” alisema Bi. Mohamed.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwashemshi,
Ezra Gweya alisema kipindi cha kilimo idadi kubwa ya wanafunzi shuleni kwake
hukimbilia mashambani jambo ambalo huathiri maendeleo ya taaluma shuleni hapo.

“Utoro hapa shuleni kwetu upo, wengine huamua
kutoa taarifa kabisa shuleni kwamba wanaandaa mashamba ya wazazi wao kwa ajili
ya kilimo...wakati mwingine ukiangalia wanasema wanategemea kilimo kwa kipato
hivyo wanalazimika kwenda mashambani,” alisema Gweya. 

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya
Bungu, Dismas Kimweli alisema kati ya Januari hadi Juni 2012 shule yake ina
jumla ya wanafunzi 226 kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne ambao ni watoro wa
kudumu.

Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya
Mlungui iliyopo Kata ya Bungu wilayani Korogwe, Sylvester Msigwa alisema idadi
kubwa ya wanafunzi watoro wanaishi peke yao kwenye ‘mageto’ hivyo kuwa na uhuru
mkubwa.

“Wanafunzi hawa huwa na uhuru kupindukia, pia wanakuwa
hawana nidhamu kwasababu wanakuwa mbali na walimu..hii ni changamoto kubwa
sana..lakini natoa wito kwa wale wanaowapangisha wanafunzi nao wabebe jukumu la
kuwalea wale watoto ipasavyo, wakiona mtoto anakwenda kinyume na maadili
wawakemee,” alisema Msigwa.

*Imeandaliwa
na Kutumwa Hapa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na
HakiElimu

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa