Home » » DC HANDENI: VITA DHIDI YA MIMBA SHULENI SI NGUVU YA SODA

DC HANDENI: VITA DHIDI YA MIMBA SHULENI SI NGUVU YA SODA

Na Arodia Peter, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, amesema mkakati aliouanzisha wa kupiga vita mimba kwa wanafunzi walioko shuleni si nguvu ya soda kama wengine wanavyodhani.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, alisema watu wa Handeni wanaliona suala la wanafunzi kuolewa au kubeba mimba ni jambo la kawaida.

Badala yake alisema ni mkakati endelevu hadi suala la mimba litakapokoma.

“Nawatangazia wazazi na wanafunzi wote wa Handeni kwamba vita hii si nguvu ya soda, ni endelevu, tumegundua watoto wa kike kubeba mimba wakiwa shuleni limekuwa ni mtindo, nasema siko tayari kuona hali hii ikiendelea.

“Katika suala hili, mtuhumiwa wa kwanza ni binti mwenyewe, wa pili ni kijana aliyempa mimba, mtuhumiwa wa tatu ni wazazi wa pande zote mbili, kwa sababu hao ndiyo wanashirikiana na kupanga mbinu za kukwepa mkono wa sheria,” alisema Muhingo.

Alisema mwaka jana pekee wanafunzi 980 waliacha shule kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kubeba mimba na mwaka huu wanafunzi wa kike 23 waliotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne wameacha shule kwa sababu ni wajawazito.

“Kwa hiyo jamii ione kwamba hali katika Wilaya ya Handeni ni mbaya, hatuwezi kuacha hali hii iendelee, hii ni vita na nimewaambia wasichana wote wanaodhani kubeba mimba ni sawa na starehe wameumia, kwa sababu watafungwa wakazalie huko gerezani,” alisema Rweyemamu.

Katika hatua nyingine, aliwataka watendaji wa Serikali wilayani humo kuhakikisha wanalipia mapema ankara za maji, umeme na simu.

Alisema baadhi yao licha ya kulipiwa gharama hizo na Serikali lakini hawataki kulipa na hivyo kukwamisha taasisi zinazotoa huduma hizo.

“Natumia nafasi hii kuwakumbusha watendaji na ofisi za Serikali wilayani kwangu kwamba wana wajibu wa kulipia gharama za umeme, simu na maji ili mamlaka husika ziweze kujiendesha,” alisema Rweyemamu.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa