Home » » WAZAZI: WAFUKUZENI WANAFUNZI WENYE SIMU

WAZAZI: WAFUKUZENI WANAFUNZI WENYE SIMU


Na Aziza Hassan, aliyekuwa Muheza
WAZAZI wa wanafunzi wa bweni wa Shule ya Sekondari Mlingano iliyopo Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wamekubali watoto wao kufukuzwa baada ya kukutwa na simu za mkononi wakiwa shuleni kwa kuwa ni kinyume cha sheria ya shule.

Maazimio hayo yalikuja wakati wa kikao cha wazazi wa wanafunzi wa bweni na uongozi wa shule, kilichofanyika juzi shuleni hapo.

Akizungumza mjini hapa juzi, Kaimu Mkuu wa Shule,  Agnes Chilongola, alisema wanafunzi walishindwa mitihani mwaka jana kutokana na upungufu wa walimu na utovu wa nidhamu, kwa kuwa wengi wamekuwa wakikamatwa wakiwa na simu bwenini.

“Tumekuwa kama askari na sio walimu, tumekuwa tukifanya misako ya kutafuta simu kwa kuwa kuna wanafunzi wengine wema wanatuambia kuwa kuna wanafunzi wana simu, unaweza kufanya msako usiipate kumbe amempa mwanafunzi wa kutwa. 

“Mwaka jana wanafunzi wamefeli sana, tulikuwa na upungufu wa walimu, kulikuwa na walimu sita lakini mwaka huu walimu waliokuwa masomoni na wengine wameajiriwa na tumefikia idadi ya walimu 18, tunaamini tatizo limeisha la walimu.

“Pia kumekuwa na utovu wa nidhamu kwa wanafunzi kutumia simu katika mabweni kwa kuwa ni kinyume cha sheria za shule na sheria inasema mwanafunzi akikamatwa na simu atafukuzwa shule, lakini tumekuwa hatufanyi hivyo,” alisema Chilongola.

Alisema mwaka jana waliwakamata wanafunzi 14 wakiwa na simu hizo ambazo zina mambo ya ajabu na kinyume cha maadili ya mwanafunzi.

“Mwaka huu tena tumewakamata wanafunzi 14 wa kidato cha nne wakiwa na simu, lakini simu hizo zimejaa mapenzi na picha za matusi na ndicho kinachosababisha mwanafunzi wengi kushindwa mitihani yao.”

Alisema wamekuwa wakipeleka majina ya wanafunzi waliokamatwa na simu katika ngazi za juu, lakini wanaambiwa wasiwafukuze na wawape adhabu za shuleni  za kawaida.

“Tumekuwa tukiwakamata na simu tunamwambia aivunje mbele ya wanafunzi wenzake, lakini imekuwa haisaidii yaani inatuumiza kwa kuwa shule imenunua simu kwa ajili ya wanafunzi, kama anataka kuwasiliana na wazazi wake anaenda kupiga simu,” alisema Chilongola. 

Kwa upande wa wazazi, walihoji kama mwanafunzi anaondoka nyumbani akiwa hana simu na shule hatoki inakuwaje anakutwa na simu.

Alisema kitendo cha wanafunzi kwenda hospitali nacho ni chanzo cha kusababisha wanafunzi kupewa simu au kununua.

Aidha, waliiomba Serikali kujenga uzio na kununua gari la shule kwa kuwa wanafunzi wanapata tabu wakiumwa ilhali shule hiyo ipo mbali na hospitali.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa