Kihistoria Mkoa wa Tanga ulitumiwa sana na wakoloni wa Kireno, Kiarabu, Kijerumani na Kiingereza ikiwa lango la biashara na uchumi kwa kuunganisha sehemu za ndani za Afrika Mashariki na Kati na sehemu mbalimbali za Dunia
kupitia bahari ya Hindi. Mwaka 1840 eneo la Manga lilikuwa njia waliopitia wafanyabiashara kutoka Bara Arabu waliokuja kutafuta meno ya tembo na watumwa. Waarabu walikuwa wakiacha vyombo vya usafiri (majahazi) eneo la Sadani (Bagamoyo) na kuanza safari kupitia Manga, Kimbe hadi Kondoa Irangi. Misafara mingine ya wafanyabiashara ilianzia Unguja kupitia Pangani, Kiwanda (Sindeni), Ngugwini, Mbego, Kwediboma, Mgera hadi Kondoa Irangi ambapo walileta nguo, shanga na vitu ili kubadilishana na pembe za ndovu, watumwa, chakula na mifungo. Kutokana na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali, wenyeji wa Tanga wamerithi tamaduni, lugha na ustaarabu wa mataifa mbalimbali ya Washirazi, Waarabu, Wachina, Wahindi, Wareno, Wajerumani, Waingereza na Waswahili.
Mkoa wa Tanga ni mzizi na chimbuko la Tanganyika kabla ya kuungana na visiwa vya Unguja na Pemba mwaka 1964 na kuunda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanganyika ilipata Uhuru mwaka 1961 huku Mkoa wa Tanga ukiwa ni msafirishaji mkubwa wa zao la Mkonge duniani na mhimili wa kukua kwa uchumi wa nchi. Jina Tanga lilitolewa na wafanyabiashara wa Kishirazi likiwa na maana nne ambazo ni Tambarare, Mabonde ya Kijani, Barabara za Milimani na Kilimo cha Milimani. Neno nyika ni la kibantu ambalo lilikuwa likitumiwa sana na wenyeji wakimaanisha mbuga au pori zaidi ya jina Tanga.
Harakati za kudai Uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza zilifanikiwa na Tanganyika kupata Uhuru tarehe 9 Disemba, 1961 chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndani ya chama cha TANU. Wakati huo (1961) Mkoa wa Tanga ulikuwa ni Jimbo lenye Wilaya tano (5) ambazo ni Wilaya ya Tanga, Handeni, Pangani, Usambara na Same
Source: Tanzania Regions Site
0 comments:
Post a Comment