Home » » WANAWAKE CHANGAMKIENI FURSA – DENDEGO

WANAWAKE CHANGAMKIENI FURSA – DENDEGO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego
WANAWAKE wajasiriamali mkoani Tanga wametakiwa kuchangamkia fursa zitakazotolewa kupitia kampeni ya ‘Mwanamke na Uchumi’ mwanzoni mwa mwezi ujao, ambapo zaidi ya wanawake 300 watanufaika na mafunzo hayo yanayotolewa na kampuni ya Angels Moment ya jijini Dar es Salaam.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego juzi, akisema kuwa fursa zitakazotolewa ni fahari kwa wanawake na wajasiriamali wa mkoa huo kwani elimu inahitajika sana wakati huu wa ushindani wa biashara.
“Fursa kama hizi mara nyingi ni nadra kuzipata na kampeni ya mwanamke na uchumi ni jibu la changamoto mbalimbali kwa wajasiriamali kwani elimu watakayoitoa ni fursa pekee ya kusonga mbele kibiashara na kiuchumi,” alisema.
Dendego aliwaomba wadau mbalimbali waendelee kujitokeza kuunga mkono juhudi za kampeni hiyo, akisema kuwa kupitia akina mama huduma zao zitaweza kufahamika na kunufaika kwa kukutana na wajasiriamali.
Nayee Mkurugenzi wa kampeni hiyo, Mahada Erick, alisema ni jawabu la changamoto zinazokumba biashara na ujasiriamali, kwamba elimu na semina zitakazotolewa zitawapa msingi wa kuanza upya kuandaa biashara.
“Kampeni hii inalenga kutoa hamasa na ari kwa akina mama kusonga mbele kimaendeleo, hakuna ubishi kuwa akina mama wana juhudi kubwa sana za kutafuta fursa za kujiongezea kipato ila tatizo ni elimu ya msingi ya kuangalia fursa zinazowazunguka na jinsi ya kuendeleza biashara zao,”alisema.
Kwa mujibu wa Erick, Angels Moment itawakutanisha akinamama waliofanikiwa kibiashara na ambao wanafanya ujasiriamali mbalimbali ili kuelezana mbinu mbalimbali za mafanikio.
Kampeni ya mwanamke na uchumi mkoani Tanga, itafanyika Novemba tano na sita katika ukumbi wa Naivera na kupambwa na msanii Linah Sanga ambaye ni balozi wa Wanawake.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa