Home » » MKAGUZI WA HESABU AFUNGWA JELA MIAKA MIWILI

MKAGUZI WA HESABU AFUNGWA JELA MIAKA MIWILI

Na Oscar Assenga, Muheza
MAHAKAMA ya Wilaya ya Muheza imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Nducha Jairos, kwa makosa 20 ya matumizi mabaya ya madaraka, huku moja likiwa la ubadhirifu wa fedha za umma.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini hapa hivi karibuni na Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Sadiki Nombo, ilisema hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Muheza, Salum Msingiti.

Alisema mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani Julai 13, mwaka huu baada ya upelelezi wa shauri lake kukamilika.

Alisema Jairos alikuwa akikusanya fedha kutoka kwa watendaji wa vijiji kwa lengo la kuwanunulia vitabu vya kutunzia kumbukumbu za hesabu bila ya kuwapatia stakabadhi.

“Alikuwa akikusanya fedha kutoka kwa watumishi na vijiji na wala hakuwa akiwapatia stakabadhi na badala yake alitumia fedha hizo kwa manufaa yake mwenyewe.

“Kwa hali hiyo mshitakiwa alihukumiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka au kulipa faini ya shilingi 500,000 na pia kutumikia kifungo cha miaka miwili kwa kosa la ufujaji na ubadhirifu au kulipa faini ya shilingi milioni moja ambapo mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hizo na kupelekwa jela,” alisema Nombo.

Aliwataka wananchi na jamii nzima kuzingatia maadili na kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Awali, akisoma hukumu hiyo, Hakimu Msigiti, alisema mshitakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kushindwa kulipa faini alizotajiwa mahakamani hapo.
Chanzo: Mtanzania

1 comments:

Anonymous said...

Nimesoma hii Comment ya Pius Jairos Nducha, leo ni miaka 3 toka aanze kutumikia kifungo chake, hebu mwandishi fuatilia maana imesikika kuwa amezuiliwa gerezani ili atumikie kifungo chake kwa Miaka 21, Kuna kutokufahamu hapo, naomba tuwasiliane kwa yeyote mwenye jibu kwa anuani hii johnsonmac2005@yahoo.com au 0784 22 77 98

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa