WALIMA MATUNDA WALILIA KIWANDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mchuuzi wa matango katika eneo la Chekereni Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro akitafuta wateja wa matunda hayo jana, ambapo alikuwa akiuza Sh1,000 kwa fungu moja lililopo kwenye bakuli

Wakulima wa matunda na mbogamboga wilayani hapa, wameiomba Serikali itekeleze ahadi yake ya kuwajengea kiwanda cha kusindika matunda ili wajihakikishie soko la uhakika.
Wakizungumza katika Kongamano la Machungwa na Matunda lililofanyika juzi, wakulima hao walisema kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika, mazao yao huozea shambani na hivyo kujikuta wakiingia hasara kubwa.
Walisema hata wapatapo soko kutoka kwa wafanyabiashara wanaowafuata vijijini, hulazimika kuyauza kwa bei ya hasara.
“Sisi wakulima wa machungwa na mbogamboga tutazidi kuwa maskini na tutaendelea kuwatajirisha wenye fedha. Tukivuna machungwa tukakaa nayo ndani zaidi ya siku tatu au nne huoza, hivyo tunalazimika kuyauza kwa bei ya kutupa ili mradi tuambulie hata fedha kidogo,” alisema Jumanne Mhina, mkazi wa Mkwaja.
Hata hivyo, Wakulima hao walihoji tatizo linalokwamisha kujengwa kwa kiwanda hicho ambacho waliahidiwa muda mrefu na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Mwenyekiti wa wakulima wa machungwa, Fikirini Juma alisema tatizo hilo linawafanya kwa sasa waendeshe kilimo hicho kama sehemu ya bustani badala ya zao la biashara kutokana na kutokuwa na faida nalo.
Alisema mbali ya kukosekana kwa soko, pia barabara ni tatizo jingine linalochangia mazao yao kuharibika
 Chanzo;Mwananchi

ASKOFU MOKIWA KUHUDHURIA MAZISHI YA JAJI LEWIS MAKAME

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Velentino Mokiwa, anatarajia kushiriki katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame,aliyefariki dunia Jumatatu iliyopita.
Hayo yalisemwa na mtoto wa mrehemu, Morris Makame, jana nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mbaramo wilayani Muheza, Tanga.

Alisema kuwa askofu huyo ni miyongoni mwa viongozi wakuu ambao watashiriki misa ya mazishi ya baba yake yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi.

Morris alisema viongozi wengine wa dini  ambao watashiriki mazishi hayo ni pamoja na Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Tanga, William Mahimbo Mndolwa na Askofu mstaafu wa Dayosisi hiyo, Philip Baji.

Alisema pia watakuwapo viongozi wa dini mbalimbali kutoka ngazi za juu  taifa na mkoa.

Morris alisema mwili wa marehemu baada ya kuwasili Muheza kutoka Dar es Salaam  utapelekwa nyumbani kwake maeneo ya Mbaramo  ambako itafanyika misa ndogo.

Alisema baada ya misa hiyo, msafara utaanza kuelekea kijijini kwao maeneo ya Tongwe wilayani na kufanyika misa kubwa ya mazishi katika Kanisa la Mtakatifu Yusuph.

Mjukuu wa marehemu, Enersti Makame, alisema kuwa kwa sasa wanafanya maandalizi ya kujenga mahema nyumbani kwake Mbaramo mjini Muheza na kijijini Tongwe.

Alisema kuwa tayari wageni mbalimbali kutoka mikoani wameshaanza kuwasili wilayani Muheza wakiwamo ndugu na jamaa.

Enersti alisema magari zaidi ya 100 ya viongozi mbalimbali yataanza kuwasili kuanzia kesho wilayani Muheza kushiriki mazishi hayo.
CHANZO: NIPASHE

MWILI WA JAJI MAKAME KUZIKWA TANGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Familia ya Jaji Lewis Makame imesema haitasahau namna jaji huyo alivyoijali na kulitumikia taifa kwa uaminifu hadi mauti yalipomfika juzi mchana.
Akizungumzia utaratibu wa maziko ya kiongozi huyo jana, mwanaye Eugene alisema kutokana na mchango wake mkubwa kwa familia na kwa taifa, watatumia siku nne ili kutoa fursa kwa familia na viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kutoa heshima zao za mwisho.
Alisema kwa sasa familia inaendelea kuratibu na kusimamia utaratibu wa awali wa maziko yake yanayotarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Tongwe Muheza, mkoani Tanga ambako alizaliwa.
“Hadi sasa tunaendelea na maandalizi ya maziko ya mzee wetu na ibada maalumu ya kumuaga itafanyika hapa nyumbani siku ya Ijumaa asubuhi kabla ya kuelekea Kanisa la St Alban na baadaye tutampeleka katika Kijiji cha Tongwe kwa ajili ya kuupumzisha mwili wake kwa amani,” alisema Eugene.
Alisema baba yake alifariki dunia juzi saa 7.45 mchana katika Hospitali ya AMI Trauma, Masaki, alikokuwa amelazwa kwa takriban mwezi mmoja.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete amemtuma salamu za rambirambi kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na familia ya marehemu kutokana na kifo hicho.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ilisema Rais amepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko, kwa kuwa ni miongoni mwa watu waliolitumikia Taifa kwa uaminifu, uadilifu, bidii na umahiri mkubwa.
Rais Kikwete alisema uongozi wake ulichangia kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa katika mazingira mapya ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
Chadema watoa salamu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nacho kimetuma salamu za rambirambi na kusema kuna haja ya kupongeza utumishi wake katika kipindi chote alichokuwa akilitumikia Taifa akiwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.
Chanzo;Mwananchi

TANGA YATAJA VITUO 3 VYA KUDHIBITI EBOLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKOA wa Tanga umetenga vituo kadhaa vya afya vitatu, ikiwa ni hatua ya maandalizi ya kudhibiti watu watakaobainika kuambukizwa virusi vya homa ya ebola.
Vituo hivyo ni cha kwenye mpaka wa Horohoro wilayani Mkinga, Masiwani Shamba na Maramba. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alibainisha hayo juzi katika mkutano na waandishi wa habari.
Alisema timu maalumu ya mkoa ya wataalamu wa afya, tayari inakagua uwezo wa vituo vingine vilivyotengwa na halmashauri nyingine za mkoa huo, kama vinastahili kupokea wagonjwa wa aina hiyo.
Alisema ingawa mpaka sasa hakuna mgonjwa wa ebola nchini, serikali imechukua hadhari hiyo, kuwaondoa wasiwasi wananchi kutokana na mwingiliano wa wageni kutoka nchi jirani kupitia mpaka wa Horohoro.
Alisema vituo hivyo vitatu vimeimarishwa kwa kupelekewa vifaa tiba, madaktari na wauguzi wenye stadi za kutosha na vitatumika kutoa huduma kwa wagonjwa watakaobainika.
“Kwa kuwa ebola haina chanjo wala tiba, mpango mkakati wa mkoa sasa ni kuhakikisha wananchi wanaelimishwa kuhusu namna ya kujikinga kuzuia maambikizi…pia tumeziagiza halmashauri zote 11 zinazounda mkoa kutenga maeneo sahihi ya kupokelea wagonjwa hao”, alisema.
Aliongeza, “wananchi ondoeni wasiwasi na tunawataka muimarishe usafi wa mazingira, hakikisheni mnanawa vizuri mikono kwa maji safi na sabuni…acheni kusalimia kwa kushikana mikono na watu kila mahali”, alisema.
Chanzo;Habari Leo

SURVEY YANG'ARA MICHUANO YA NANENANE TANGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Timu ya Survey Veterani ya jijini Dar es Salaam imeifunga timu ya Kombaini Vijana ya jijini Tanga kwa mabao 2-1, katika mchezo wa kuazimisha Siku ya Wakulima (Nanenane) kwenye viwanja vya Disuza, vilivyopo mkoani hapa.

Mchezo huo ambao ulidhaminiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ulikuwa na lengo la kukutanisha timu za maveterani ili kujenga mshikamano na kuhamasisha watu kupenda michezo nchini.
Katika mchezo huo, mchezaji wa Survey, Carlos Mdinga alijifunga wakati akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na wapinzani hatua ambayo ilisababisha kuzaa bao dakika ya pili.
Hata hivyo katika mchezo huo timu ya Survey ilionyesha makali yake, kwani dakika ya 40 walisawazisha bao hilo kupitia kwa kiungo wake, Silyvester Malango.
Bahati ilizidi kung’aa kwa timu ya Survey Veterani baada ya kupata bao la pili dakika ya 70, lililowekwa wavuni na mshambuliaji David Emmanuel na hivyo kuibuka na ushini wa mabao 2-1.
Katika mchezo mwengine, Best point veterani iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya kombaini ya wazee ya jijini Tanga.
Mabao ya Best Point yalifungwa na Sadiki Salumu (7) na Miraji Paulo katika dakika za mwisho za mchezo huo.
Baada yakumalizika kwa mchezo huo, kocha Seleman Mgaya, ambaye ni Katibu wa Survey Veterani ya Dar es Salaam, alisema wamefurahishwa na ushirikiano unaotolewa na mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) hasa kwa kuonyesha mchango wao katika michezo.
“Tunaishukuru NSSF kwa moyo wa kutukutanisha pamoja kimichezo, hatua ambayo tunajivunia kwani wao wametambua umuhimu wetu, hivyo hatuna budi kutoa ushirikiano,” alisema Mgaya.
Chanzo:Mwananchi

ATAKA ELIMU YA UJASIRIAMALI WA VIKUNDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
SERIKALI imetakiwa kuvipa  kipaumbele  vikundi vya ujasiriamali ikiwa na pamoja na kuwapatia elimu ya mafunzo mara kwa mara.
 Ushauri huo ulitolewa na Mwalimu wa Vikoba, Rukia Mwinyi wakati wa mafunzo ya wajasiliamali yaliyofanyika jana jijini Tanga, akisema kuwa endapo serikali itaweza kutoa elimu hiyo ipasavyo ile sera ya kupambana na umasikini itafanikiwa.
 “Jambo hili likifuatiliwa kwa umakini tutafanikiwa kujikomboa katika umasikini kwani wajasiriamali waliowengi hasa katika vikundi vyetu hatuna elimu hii kwa ufasaha ambayo tunaihitaji kwa nguvu zote,”alisema Rukia.
 Aidha, Rukia alisema mafunzo kwa wajasiriamali yamekuwa hayatolewi mara kwa mara kitendo kinachowafanya kutokuwa na uelewa sahihi juu ya suala hilo na kushindwa kutimiza malengo waliokusudia.
 Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego aliwataka kuwa na uchungu na maendeleo ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa za kimaendeleo wanazozifanya ili kufikia lengo la kuongeza pato la mtu mmoja mmoja.
 Dendego alisema mbali na kutangaza bidhaa zao pia wajikite katika shughuli za kilimo ambazo wataziuza nje ya nchi hususani Kenya ambako wamekuwa na uhitaji mkubwa wa mazao kama chakula yatayopatikana mkoani Tanga.
 Chanzo:Tanzania Daima

MLINGANO WAPATA KITUO CHA AFYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
SHIRIKA la Kikorea la kuhudumia afya za watoto chini ya miaka kumi (UHIC), kupitia mradi wake wa Keeper, limefungua kituo cha afya katika Kijiji cha Mlingano, Muheza mkoani Tanga.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, alisema kituo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa eneo hilo kutibu watoto wao kwa haraka pindi wanapopatwa na maradhi mbalimbali.
Alisema nia ya serikali ni kuhakikisha wananchi wake hawatembei umbali mrefu kufuata huduma za kijamii ikiwemo vituo vya afya, hivyo uamuzi wa kuweka kituo eneo hilo ni wa busara na utawapunguzia wananchi kwenda umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
“Niwapongeze UHIC kupitia Shirika la Kimaendeleo la Korea ya Kusini (Koica), kwa kuweza kubuni mradi huu wa kutoa tiba kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10, utasaidia kuboresha afya za watoto wengi kwenye wilaya hii, hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini,” alisema Mgalu.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Koica, Kim Seung Bum, alisema kuwa afya bora kwa mtoto chini ya miaka kumi ni muhimu katika kujiletea maendeleo endelevu kwa ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rashid Iddi, aliiomba serikali kuharakisha kupeleka huduma ya umeme kwenye kituo hicho ili kiweze kutoa huduma muda wote badala ya sasa ikifika jioni hulazimika kufungwa
Chanzo;Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa