Home » » BUMBULI WAMPONGEZA WAZIRI MAKAMBA NI BAADA YA SERIKALI KUVUNJA MKATABA NA MWEKEZAJI WA KIWANDA CHA KUZALISHA CHAI MPONDE

BUMBULI WAMPONGEZA WAZIRI MAKAMBA NI BAADA YA SERIKALI KUVUNJA MKATABA NA MWEKEZAJI WA KIWANDA CHA KUZALISHA CHAI MPONDE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Wananchi waishio maeneo mbalimbali katika Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga wamempongeza Mbunge wa Bumburi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba kwa hatua ya kuwasaidia kuishawishi serikali kukipatia ufumbuzi mgogoro wa kiwanda cha chai cha Mponde. 
Wnanchi wakimpongeza Mbunge wa Bumburi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba

NA RAISA SAIDI, BUMBULI. 
SERIKALI ya Tanzania imevunja rasmi mkataba na mwekezaji wakiwanda cha kuzalisha Chai cha Mponde kilichopo wilayani Bumbuli Mkoani Tanga na kuamuru kitwaliwe na kianze kazi mara moja. 
 Akizungumza katika mkutano uliowajumuisha wadau wazao la chai,Msajili wa Hazina Laurence Mafuru amesema kuwa kwa mamlaka aliyopewa amevunja rasmi mkataba huo kwasababu Mwekezaji aliyekuwepo kashindwa kutekeleza makubaliano yaliyoweka . 
 Mafuru alisema kuwa wamefikia uwamuzi huo kutokana na kujiridhisha pamoja na kupitia mikataba walioingia na mwekezaji huyo ndipo serikali imeamua ikirudishe kiwanda hicho mikononi mwa Wizara ya Viwanda na Biashara ili utaratibu mpya wa uendeshwaji wa kiwanda uanze huku Bodi ya Chai Tanzania ukiendelea kukisimamia mpaka hapo serikali itakapotafuta mwekezaji mwingine. 
 Mei mwaka 2013, wakulima wa chai waliitisha mkutano na kumwalika Mbunge wa Jimbo la Bumbuli Januari Makamba na kueleza kutokuwa na imani na mwekezaji na Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (UTEGA) na kuamua kukifunga kiwanda licha ya Mbunge kuwasihi wasichukue uamuzi huo wa hasira. 
 Tangu wakati huo jitihada nyingi zimefanyika zikiongozwa na Mheshimiwa Makamba kuhakikisha kwamba kiwanda kinafunguliwa na wakulima wanauza chai yao. 
"Tuliteseka kwa muda mrefu na leo Serikali imefanya uamuzi wa kukirudisha kiwanda mikononi mwetu, Tunaishukuru Serikali kwa kutusaidia sisi wananchi tulioteseka kwa muda mrefu ,” Alisema Challes Ngovi ambaye ni mkulima wa chai Mponde. 
 Hata hivyo Mafuru alibainisha kuwa ucheleweshaji wa kukifungua kiwanda hicho ulitokana na utaratibu uliokuwa ukifanywa na Serikali na baada ya kujiridhisha ndipo ikaamua kumuandikia rasmi barua Mwenyekiti wa Utega inayoonyesha kuvunjwa kwa mkataba huo na kuamuru kiwanda kirudi Serikalini. 
 Kwa upande wake, Mbunge wa Bumbuli January Makamba alisema kwamba kazi waliyomtuma wananchi ya kukirudisha kiwanda mikononi mwao imekamilika ingawa imechukua muda mrefu. Makamba ambaye pia ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughuliokia Mazingira na Muungano alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Magufuli kwa kuingilia kati mgogoro huo ambao umedumu kwa zaidi miaka mitatu na hatimae kuumaliza. 
Wakati huo huo,Wananchi waishio maeneo mbalimbali katika Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga wamempongeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira kwa hatua ya kuwasaidia kuishawishi serikali kukipatia ufumbuzi mgogoro wa kiwanda cha chai cha Mponde. 
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, mmoja ya wakulima hao,Swahiba Mbili alisema kuwa kufunguliwa utawasaidia wananchi ambao walikuwa na changamoto ya mazao yao kuharibika shambani kupata soko la uhakika ambalo linaweza kuwainua kimaisha. 
 Swahiba alisema kuwa wao kama wakulima pamoja na kuishukuru serikali kutwaa kiwanda lakini wanamshukuru Januari Makamba kwa sababu hakuweza kuwa mbali nao kwenye kipindi chote wakati kiwanda hicho kimefungwa na kuaidi kumpa ushirikiano katika kipindi cha kuwatumikia wananchi hao.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa