Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
INAKADIRIWA kuwa watu milioni 270 wanahusika na ajali za kemikali
maeneo ya kazi, huku milioni 160 wanasumbuliwa na magonjwa yatokanayo
na athari za kemikali kila mwaka kati ya watu bilioni 2.8 wanaofanya
kazi duniani kote.
Takwimu hizo ni kwa mujibu ya Shirika la Kazi Duniani (ILO)
zilizotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samweli Manyele wakati
akifungua mafunzo ya wadau juu ya usalama wa kemikali bandarini na
wakati wa usafirishaji iliyofanyika mkoani hapa jana.
Alisema kutokana na takwimu hizo, Serikali ya Tanzania ipo kwenye
mkakati wa kuchukua hatua ikiwemo kutoa mafunzo kwa wasafirishaji ili
kuhakikisha wanapunguza athari zinazosababishwa na kemikali za
viwandani.
“Nchi yetu ina matumizi makubwa ya kemikali aina ya Ammonium
Nitrate ambayo ina asili ya kulipuka, na inatumika kwenye mbolea ili
kuongeza uzalishaji na kemikali nyingine zenye athari zinazotumika
kwenye viwanda.
“Ipo haja ya makusudi kuhakikisha usafirishaji wake hauleti athari
kwa binadamu na viumbe wengine,” alisema Profesa Manyele na kuongeza
kwamba baadhi ya matukio yaliyo nje ya utaratibu ulioruhusiwa wa
tindikali yamesababisha athari kwa watu tisa kwenye mikoa ya Dar es
Salaam, Mwanza na Zanzibar mwaka 2013.
Alisema mwaka huu ilihusisha matukio ya ajali za magari kupinduka
wakati wa usafirishaji tindikali maeneo ya Morogoro na Dar es Salaam
ambapo ilidhibitiwa hivyo haikuleta athari.
Profesa Manyele alisema katika kudhibiti athari za kemikali,
serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanza mchakato wa
kuwa na kituo cha kuratibu na kudhibiti athari za sumu ili kutoa msaada
wa haraka katika matukio ya sumu na ajali zinapotokea.
“Mpaka Julai mwaka huu tutakuwa tumetoa kanuni mpya ambazo
zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa ili kulinda eneo la usafirishaji na
makampuni yanayojihusisha na usafirishaji wa kemikali hizo kuwa
salama,” aliongeza mkemia huyo.
Mkurungezi wa Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali, Sabanitho Ntega,
alisema mafunzo hayo yamewalenga wafanyakazi wa bandarini kwani ndio
lango kuu la kupitisha kemikali kutoka nje ya nchi kwa ajili ya
matumizi ya viwanda.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment