Home » » Utapiamlo; tatizo sugu linalotesa wengi Kilindi

Utapiamlo; tatizo sugu linalotesa wengi Kilindi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
 Makombo Hatibu  akimlisha uji wa lishe mtoto Hatibu Abdallah, kushoto ni mtoto Asha Abdalah hivi karibuni mkoani Tanga

Kwenye duka mojawapo lililopo katika eneo la Mgera wilayani Kilindi mkoani Tanga, nakutana na mama mwenye mawazo mengi, mkononi amewapakata watoto wawili ambao wanalia muda wote.
Mmoja wao ana tumbo kubwa na mwingine amepauka uso, nywele zimelainika kwa kiasi kikubwa.Hali ile ilinishtua na kunilazimu nimsogelee mama yule ili kujua tatizo gani linalomsumbua yeye na watoto wake.
Kwa upole alinijibu kwa kuanza kunieleza kuwa watoto wake wanalia kutokana na njaa na kwamba wanakula mlo mmoja na nyakati za asubuhi anawalisha viporo
Mama huyo, Mwamvua Bakari anasema watoto wake wamegundulika kuwa na utapiamlo baada ya Kikundi cha Afya na Lishe, Mama Mjamzito na Mtoto kilichopo Mgera kumtembelea nyumbani kwake na kubaini watoto wake wanalo tatizo hilo.
Hayuko peke yake, wapo kinamama na watoto wengi zaidi wenye tatizo kama hilo wilayani Kilindi na Mkoa wa Tanga kwa jumla.
Hata hivyo, serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta mbalimbali za huduma ya afya, mama na mtoto kupitia Shirika la World Vision wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapungua nchini.
Kutokana na jitihada hizo, wameweza kupunguza idadi kubwa ya watoto wanaokufa kwa utapiamlo nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Mwanamvua kwa upande wake anaeleza kuwa kuanzia mwaka 2010 wakati alipojifungua mtoto wake wa kwanza maisha yake yalikuwa magumu kutokana na umaskini unaoikabili familia yao.
Anasema mume wake amekuwa akitegemea zaidi vibarua vya kulima ili apate fedha ya kununulia walau kibaba cha unga na wakati mwingine hulazimika kulala na njaa.
“Tatizo kubwa ni kuwa mimi na mume wangu hatuna kipato, hivyo nilianza kuwaacha watoto wa miezi tisa nyumbani bila chakula. Kwa sasa, mmoja ana miaka mitatu na mwingine mitano, wote nilikuwa nikiwaacha kwa bibi yao nao walikuwa wanakunywa uji asubuhi hadi jioni tutakaporudi kutoka kwenye mahangaiko,” anasema.
Anaeleza kuwa maisha yao yalipokuwa magumu zaidi, walilazimika kununua nusu kilo ya unga ambao haukutosha, kiasi kwamba walikula mlo mmoja kwa siku na kulazimika kuacha kiporo ili watoto wanapoamka asubuhi waweze kula.
Baada ya kikundi hicho kuwatembelea nyumbani kwao walimweleza aende kliniki kwa ajili ya kupima uzito wa watoto hao. Mtoto wa miaka mitatu alikutwa na uzito wa kilo 11.3 na yule mwenye miaka mitano akiwa nazo kilo 10.3 pia.
Mama mwingine mwenye watoto pacha wenye miaka miwili aliyejitambulisha kwa jina la Makombo Hatibu anasema watoto wake aliwaanza kula kiporo cha ugali wakiwa na umri wa miezi sita.
Anasema inategemea siku hiyo kama unga umebaki kidogo anawapikia uji kama hakuna siku hiyo analazimika kumsubiri mume wake hadi hapo atakaporudi jioni ili wapike chakula.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Afya ya Lishe, Mama Mjamzito, Muya Atanasia anasema waliwabaini watoto hao wakati wanapita nyumba kwa nyumba wakitoa elimu ya lishe.
Anasema baadaye waliwachukua wazazi hao kwa ajili ya kutoa elimu ya lishe bora ili waweze kujifunza jinsi ya kutengeneza lishe isiyokuwa na gharama kwa kutumia mazao wanayolima kijijini hapo.
Anaelezea kikundi chao kinawakusanya watoto wote waliopata utapiamlo kwa kuwapikia uji wa lishe uliochanganywa na karanga, mchele, ulezi na maharage wakati huo wanawaelekeza wazazi wao jinsi ya kuandaa vyakula hivyo.
“Baada ya kunywa uji huo tunawapa tunda huku uji mwingine tunawaelekeza wazazi wao waweke kwenye chupa kama chakula kimechelewa ili waweze kunywa.
“Kwa kupunguza gharama ya ulezi, mara nyingi tunawashauri jamii watumie mahindi ya lishe yaliyochanganywa na maziwa kwa ajili ya kupunguza gharama kulingana na maisha wanayoishi kijijini huku,”anasema.
Anaongeza kuwa mara nyingi wanaelekezwa kutumia vipimo zaidi wakati huo wakisisitiza uji huo unapoandaliwa unawekwa sukari na chumvi wakati wa kuandaa lishe ya watoto hao.
Anaeleza kuwa watoto hawapati muda mzuri wa kunyonya, hivyo wazazi wao walikuwa hawatambui kuwa viporo kwa mtoto chini ya umri wa miaka mitano husababisha utapiamlo.
Hawazingatii muda wa kula. Wanakwenda shamba na wanaporudi jioni ndipo huandaa chakula cha watu wazima na kuwapa watoto wao bila kujali muda.
“Chakula kikuu wanachopikiwa watoto hao ni ugali na mlenda na baadaye huwaacha watoto wenyewe wale wenyewe. Kwa mfano kama watoto hawa wawili pacha tumewakuta katika hali mbaya ,” anasema mratibu huyo.
Katibu wa kikundi hicho, Mwajabu Mrisho anasema ndani ya siku saba watoto hao waliongezeka uzito. Yule mwenye miaka mitano aliyekuwa na kilo 10.3, aliongezeka na kufikia kilo 11.9 huku mwenye miaka mitatu aliyekuwa na kilo 11.3 hakuongezeka uzito kwa sababu alikuwa na minyoo pamoja na malaria.
Anasema kwa watoto wale pacha, yule wa kike alikuwa na uzito wa kilo 6.5 aliongezeka na kufikia kilo 7.1 na yule wa kiume aliyekuwa na kilo 5.9 aliongezeka na kuwa na kilo 6.8.
Mwajabu anasema wamefanikiwa kutoa elimu ya afya ya mama mjamzito na mtoto, hivyo kutokana na elimu hiyo wanaume wameanza kuwasindikiza wake zao hadi vituo vya afya na hata kujaribu kuwashawishi wake zao kuhudhuria kwenye kliniki mara kwa mara.
Mpango wao kwa mwezi Desemba mwaka huu utatoa elimu katika vijiji vya Jungu, Makingo, Kwendiswati pamoja na Lekiting’e ambapo awamu ya kwanza elimu hiyo ilitolewa kwenye vijiji vya Mgera, Balang’a na Kisangasa na kwamba uhamasishaji utaongezeka.
Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Kata ya Kibirashi, Augustino Semzige anasema kupitia mradi huo, umesaidia kupunguza ugonjwa huo kwa asilimia 75. Miaka ya nyuma uliongezeka kwa asilimia 95 kwa sababu ilitokea njaa kubwa wilayani hapo.
“Mradi huu wa Afya, Mama na Mtoto iongeze nguvu kwa suala la utapiamlo, hasa kuielimisha jamii ili waweze kujua jinsi ya kuandaa lishe ya mama mjamzito na mtoto. Kama mama mjamzito akikosa virutubisho wakati wa mimba anaweza kupata upungufu wa damu na kusababisha kuvimba miguu na uso ambapo anakuwa hana nguvu ya kumsukuma mtoto wakati wa kujifungua,” anasema Dk Semzige
Pia, ushiriki wa wanaume kupitia mradi huo umesaidia kwa asilimia 95 walioanza kuhudhuria kliniki wakiwa na wake zao. Hivyo mwanamume anapogundua kuwa mke au mama ana matatizo, anakuwa mstari wa mbele kumpeleka kwenye kituo cha afya.
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Wilayani Kilindi, Ruth Ligubi anasema zaidi ya wanaume 6,197 wamekuwa wakishirikiana na wake zao baada ya kupata elimu ya lishe kwa mama mjamzito na mtoto. Kupitia mradi huo, huwajali familia zao na kuzipa kipaumbele lishe bora na kumjali mama mjamzito.
“Wanaume waliokuja na wake zao kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2013 walikuwa 6,197 ukilinganisha na miaka ya nyuma walipokuwa hawazidi 30. Hivyo kwa sasa uelewa umekuwa mkubwa,” anasema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Dk Shemdaa Ngereza anasema tatizo la utapiamlo ni kubwa hasa kwenye maeneo ya vijiji vya ndani kutokana na kipato kidogo cha fedha cha kuandaa lishe.
Anasema asilimia 4.5 ya watoto waliougua utapiamlo, imepungua kutokana na elimu inayotolewa na mradi wa Afya, Mama na Mtoto kupitia World Vision.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa