Home » » TAMKO RASMI LA BAVICHA MKOA WA TANGA KUHUSU KATIBU WA BAVICHA MKOANI WA TANGA BW DEOGRATIAS KISANDU

TAMKO RASMI LA BAVICHA MKOA WA TANGA KUHUSU KATIBU WA BAVICHA MKOANI WA TANGA BW DEOGRATIAS KISANDU



NAPENDA kutoa taarifa kwa umma kutokana na habari zinazoandikwa kwenye  baadhi ya vyombo vya habari, huku chanzo cha habari hizo kikiwa ni Katibu  wa BAVICHA Mkoa wa Tanga, Bwana Deogratias Kisandu, ambazo zimekuwa  zikionesha kuwa vijana wa Mkoa wa Tanga tuna walakini katika chama chetu  cha CHADEMA. 

Leo katika baadhi ya vyombo vya habari, Bwana Kisandu amenukuliwa akitoa  taarifa kuwa yeye pamoja na makatibu wenzake nchi nzima, wamepanga kufanya  maandamano ya kuupinga uongozi wa juu wa kitaifa wa BAVICHA. 

Kwa kutambua na kuheshimu kuwa moja ya misingi muhimu ya uendeshaji wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na mabaraza yake ni  vikao, ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba, miongozo, taratibu, kanuni na  itifaki za chama, vijana wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, ambao mimi ndiye msemaji  wao kikatiba, tunaamini Bwana Kisandu anazidi kupotoka. 


Kwa hiyo basi, kama ambavyo nimeshapokea malalamiko kutoka kwa vijana wa  Tanga baada ya hatua yake ya awali ya Bwana Kisandu kutoa taarifa kwa  vyombo vya habari, bila kuzingatia katiba, maadili na itifaki ya chama,  akibeba propaganda nyepesi za Sekretarieti ya CCM, juu ya suala la kadi  mbili kwa Katibu Mkuu wetu Dkt. Willibrod Slaa, kuna haja ya kufanya vikao  kuangalia na kujadili mwenendo wa kiongozi mwenzetu huyo. 


Kwa sababu kama vijana makini wa CHADEMA, chama ambacho kinaamini katika  kutoa utumishi bora, mikakati madhubuti, sera imara kwa ajili ya maendeleo  endelevu ya Watanzania wote, ambao wamekosa uongozi bora na siasa safi  kutokana na ufisadi na ubadhirifu wa CCM, lazima tuwe makini na kila  mwenzetu yeyote yule ambaye anaonekana kufanya kazi ya CCM kwa kutumia jina  la CHADEMA. 


Tunapenda kumkumbusha Bwana Kisandu kuwa atumie muda wake pia kuisoma vyema
katiba ya CHADEMA hasa katika Sura ya 10 inayozungumzia Maadili ya  Viongozi, Sifa mahususi za viongozi na maadili ya wanachama, kifungu

10.1(1-13), toleo la mwaka 2006. 

Kuhusu masuala ya ushiriki wa vijana kwenye shughuli mbalimbali za chama  ikiwemo mikutano ya M4C, Bwana Kisandu anapaswa kuelewa kuwa vijana  kutokana maeneo mbalimbali ya nchi, ukiwemo Mkoa wa Tanga tumekuwa  tukishirikishwa, kupitia utaratibu maalum unaopangwa na Ofisi ya Katibu  Mkuu, ambao tunaamini mpaka sasa umetoa fursa kwa wanachama wote, wakiwemo  wazee, wanawake na vijana kukieneza na kukiimarisha chama maeneo mbalimbali  ya nchi. 

Na maamuzi yote ya msingi kwa uendeshaji wa Baraza hasa kwa Mkoa wa Tanga  yatafanyika kupitia vikao na hatua zitachukuliwa kwa kufuata katiba,  kanuni, maadili, itifaki na miongozo ya chama. 

 *Aron J Mashuve* 
*Mwenyekiti wa BAVICHA* 
*Mkoa Wa Tanga*

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa