MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Uwasa) imesema
inasubiri kupata kibali cha dharura kutoka kwa Wakala wa Manunuzi wa
Serikali (GPSA) kukarabati mtandao wa majitaka katika baadhi ya maeneo
ambayo yanahatarisha afya za wakazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga- Uwasa, Joshua Mgeyekwa amebainisha hayo
jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu mchakato wa
uzibuaji wa mtandao wa majitaka katika maeneo mbalimbali ya jiji na
kusema lengo ni kutatua changamoto hiyo.
Aliyataja maeneo yatakayohusika na ukarabati kuwa ni Usagara,
barabara ya Swahili pamoja na barabara za 11, 12, 13 na 14 Lumumba
ambayo mabomba yake ya kupitisha majitaka yamevunjika kutokana na mvua
za masika zinazoendelea kunyesha msimu huu.
“Mvua zinazoendelea kunyesha zimefanya udongo uelemee mabomba ambayo
yamechakaa kutokana na asili ya kemikali zilizomo kwenye majitaka …na
kwakuwa yametengenezwa kwa ‘Asbestos’ kumefanya mabomba husika kuvunjika
na kuziba hatua ambayo inazuia majitaka kutiririka vizuri na badala
yake huzagaa mtaani na kuhatarisha afya za wakazi. Ili kupata ufumbuzi
wa tatizo hili tayari mamlaka imeomba kibali cha manunuzi ya dharura kwa
wakala wa manunuzi GPSA kwa ajili ya kupata mkandarasi mwenye mitambo
ili kwa haraka afanye ukarabati huo ambao tunaamini utarejesha mfumo
katika hali ya kawaida”, alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa wavumilivu kwa kuchukua tahadhari
zinazostahili hasa wakati huu ambapo Uwasa inafanya udhibiti wa muda wa
majitaka.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment