Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MRADI wa kusambaza mitambo ya bayogesi ngazi ya kaya nchini (TDBP),
umetoa Euro 100,000 (Sh milioni 230) kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha
Wafugaji Ng’ombe wa Maziwa cha Mkoa wa Tanga (TDCU).
Mratibu wa TDBP, Lehada Shila amesema fedha hizo, zitatumika
kutengeneza mfuko wa mzunguko wa kutoa mikopo ya masharti nafuu ili
kuwawezesha wanachama wa TDCU wakope na kununulia mitambo ya bayogesi
inayoratibiwa na TDBP.
Alisema hayo katika sherehe za kuzindua awamu ya pili ya mradi huo,
zilizofanyika Kijiji cha Boza Wilaya ya Pangani mkoani Tanga hivi
karibuni, ”Kwa kujua umuhimu wa mitambo ya bayogesi katika kuleta
mapinduzi ya kilimo na viwango vya maisha miongoni mwa wakulima nchini,
Serikali za Tanzania na Norway kupitia Wakala wa Nishati Vijijini umetoa
fedha za kuwapatia punguzo la bei ya mitambo ya bayogesi la takribani
Sh 240,000 kwa kila mtambo unaolipiwa na mkulima, hivyo kumfanya alipe
Sh 960,000 tu badala ya bei ya awali ya Sh milioni 1.2,” alieleza Shila.
Mratibu huyo aliwahimiza wafugaji wa Mkoa wa Tanga na mikoa mingine,
ambayo pia ni sehemu ya walengwa wa kujenga mitambo 10,000 ndani ya
miaka miwili, kuhakikisha wanaitumia fursa hii ya unafuu wa kulipia
gharama za mitambo na hasa punguzo hili la bei, inayolipiwa na Wakala wa
Umeme Vijijini (REA).
Akizindua mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza
aliyewakilishwa na Ofisa Uvuvi na Mifugo, Archie Mntambo alielezea
kufurahishwa kwake na uamuzi wa serikali kupitia REA kutoa Sh Sh bilioni
3.06 kutumika kutoa punguzo miongoni mwa watumiaji wa mitambo ya
biogesi nchi nzima.
“Kwa kutoa fedha hizi ili kuwapa nafuu watumiaji wa nishati itokanayo
na mitambo ya bayogesi, huu ni uthibitisho tosha serikali yetu
inawajali wafugaji na inafanya kila juhudi kuona kuwa wanaboresha
viwango vya maisha na hivyo kufanikiwa kujitoa katika lindi la umasikini
wa kupitiliza. “Lakini jambo lingine lililonivutia zaidi ni kwa
marafiki zetu wa Serikali ya Uholanzi kutoa Sh bilioni sita ili
kutekeleza mradi huu, hii ni ishara kuwa mataifa yetu haya ni rafiki na
yanajikita katika kuona kuwa maisha ya Watanzania yanaboreshwa zaidi na
zaidi,” alisisitiza mkuu huyo wa mkoa.
Mkulima na mfugaji, Elibariki Kishia (74) aliyejenga mtambo wake kwa
Sh 980,000 wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya TDBP kati ya
mwaka 2009 hadi 2015, alisema mtambo huo umebadili maisha yake, kwani
mazao anayozalisha shambani yameongezeka kutokana na kutumia mbolea bora
itokanayo na kinyesi cha ng’ombe, kilichochakatwa katika mtambo wa
biogesi.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment