Home » » ‘GAIDI’ WA AMBONI TANGA MBARONI

‘GAIDI’ WA AMBONI TANGA MBARONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI la Polisi mkoani Tanga, limedai kufanikiwa kumkamata mmoja wa watuhumiwa aliyehusika kwenye tukio lenye sura ya kigaidi katika mapango ya Amboni.
Zaidi Jeshi hilo limemuhusisha mtuhumiwa huyo na tukio la uporaji silaha kwa askari waliokuwa doria eneo la barabara ya nne na tano Mtaa wa Makoko jijini Tanga, Januari 26 mwaka huu.
Takribani mwezi mmoja uliopita, tukio hilo la Amboni ambalo msingi wa kujulikana kwake ulitokana na kuporwa kwa silaha hizo, lilisababisha mapambano makali ya kurushiana risasi kati ya polisi wakishirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi au magaidi waliokuwa wamejificha katika mapango ya Amboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 18 mwaka huu saa mbili usiku katika eneo la Kabuku huku akiwa na bunduki yenye risasi 29.
Ndaki alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kumekuja baada ya jeshi hilo kupata taarifa za siri kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo walimuhoji ambapo mbali na kukiri kuhusika katika kupora silaha, pia alikiri kuwa ni miongoni mwa wanaounda kundi hilo lililokuwa limejificha katika mapango hayo yaliyoko katika Kijiji cha Mleni.
Kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa huyo alikiri kuwapo ndani ya mapango hayo wakati wa mapambano baina yao na Jeshi la Polisi na kwamba alikuwa ni mtu wa mwisho kutoka katika mapango hayo akiwa na bunduki moja iliyokuwa imefichwa.
Kaimu Kamanda huyo alisema Machi 19 mwaka huu baada ya mtuhumiwa
huyo kukamatwa, saa mbili asubuhi aliwaongoza askari wa kikosi kazi Taifa wakiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Tanga (RCO) kwenda kuwaonyesha silaha hiyo.
Alisema baada ya kufika katika mapango hayo walionyeshwa bunduki moja aina ya SMG yenye namba 14303545 ikiwa na risasi 29 ambayo ni miongoni
mwa silaha zilizoporwa askari Januari 26 mwaka huu.

Alisema mtuhumiwa huyo pia aliwaonyesha panga moja, begi moja la kahawia likiwa na nguo mbalimbali na mabomu matatu ya kutengeneza kienyeji vifaa ambavyo walikuwa wakivitumia wakati wa mapambano kati yao na polisi waliokuwa wakisaidiwa na JWTZ.
Aliongeza kuwa kupatikana kwa silaha hiyo kunafanya silaha zote mbili walizoporwa askari wa Jeshi hilo ambao walikuwa doria kupatikana.

Chanzo:Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa