Home » » SHIMO LA TAMBIKO LILIVYOGEUKA ‘JEHANAMU’ HANDENI

SHIMO LA TAMBIKO LILIVYOGEUKA ‘JEHANAMU’ HANDENI


Aziza Hassani akimuuguza mtoto wake Zuhura Rajabu (17) aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, baada ya kuungua mwili mzima walipokuwa wakifanyiwa dawa kwa mganga wa kienyeji na mama huyo alipata majeraha madogo kichwani. Picha na Rajabu Athumani.  

“Ama kweli hujafa hujaumbika,” walisema walimwengu wakiwa na maana kubwa kwamba tangu kuzaliwa hadi kufa hupitia au kukumbwa na mabadiliko mbalimbali, lakini litakavyotokea au lini ni siri ya Mungu pekee.
Binadamu anaweza kuzaliwa bila kasoro yoyote na kujijengea matumaini ya kutimiza malengo yake bila wasi wasi, lakini akapatwa na mkasa utakaofuta ndoto zake zote.
Hivi ndivyo ilivyotokea kwa msichana Zuhura Rajab mwenye umri wa miaka 17, ambaye kwa mfumo wa maisha ya Kitanzania hajatimiza ndoto yake hata moja, awe akiishi kijiji au mjini kwani hajafikisha umri wa kujitegemea.
Mbali na ukweli huo, maisha na ndoto za Zuhura zimefifia ghafla baada ya kuingizwa na babu yake kwenye imani iliyogharimu maisha yake na sasa anauguza majeraha kutokana na kuungua moto huku wataalamu wakisema asilimia 72 ya mwili wake umeathirika kwa moto.
Mkasa uliomkuta Zuhura hataweza kuusahau maishani mwake kwani maelezo ya kitaalamu yanaonyesha kuwa akipona, asilimia chache ya viungo vyake vitaweza kufanya kazi kwa usahihi kwani majeraha ya moto husababisha ngozi kujikunja.
Ilivyotokea
“Mimi na wanangu tuliitwa nyumbani, tulifika kwa mganga mimi, mama yangu mzazi pamoja na watoto wangu wawili. Sisi ndiyo tuliingizwa kwenye shimo, ila baba hakuingia bali alibaki juu na yule mganga. Hadi tukio linatokea, hakusogea kabisa kwenye lile shimo.”
Ndivyo anavyoanza kusimulia Aziza Hassani (35) mama wa watoto wawili ambaye yeye na mtoto wake mmoja wamepona kwenye tukio hilo la moto uliowashwa kwa makusudi na mganga wa kienyeji nao kuambiwa watoke huku moto ukiwaka na atakayeshindwa, atakuwa amekamatwa na dawa ya mganga huyo.Anasimulia kwamba November 26 alipigiwa simu na mama yake mzazi aliyemweleza kuwa kuna dawa (tambiko) la wanafamilia hivyo yeye na wanawe kutakiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya shughuli hiyo.
Anaeleza kuwa alifika nyumbani mapema siku hiyo hiyo akiitika wito wa wazazi wake na kuelezwa kwamba anapaswa kushiriki kwenye dawa kesho yake Novemba 27, agizo ambalo alikubaliana nalo, lakini alipouliza ni dawa ya nini alielezwa kuwa ni tambiko.
Aziza anaeleza kuwa walifika kwa mganga huyo na kuanza kufanyiwa dawa iliyofanyika ndani ya shimo ambalo liliezekwa kwa nyasi kavu juu yake na kuachwa nafasi ndogo mfano wa mlango, ambao ndiyo walioutumia kuingilia ndani yake na dawa ilifanyika.
“Mganga alianza kufanya kazi yake sisi tukiwa ndani ya shimo. Tulikuwa mimi mtoto wangu mdogo Hassan Rajab (4), Zuhura Rajabu (17) pamoja na mama yangu mzazi, Hadija Abdallah(65) ambaye ndiye aliyeniita katika dawa hiyo,” anasema Aziza.
Anafafanua kuwa iliwachukua zaidi ya nusu saa wakiwa ndani ya shimo hilo hadi hatua ya mwisho ya dawa hiyo na walimwona mganga huyo akiwa amemaliza kufanya mambo yake na kubaki pembeni ya shimo walilokuwamo.

Baada ya muda walidhani mganga ameshamaliza na kumuuliza wanaweza kutoka, lakini aliwajibu dawa bado inaendelea na ghafla mganga huyo aliwasha moto juu ya zile nyasi.
“Moto mkubwa ukaanza kuwaka ndipo mganga akatuamrisha tutoke shimoni huku moto ukiendelea kuenea hadi mlangoni,” Aziza anasimulia kwa uchungu.
Anasema kuwa baada ya kauli hiyo ya mganga kuwa waanze kujiokoa, alianza kumrusha nje mtoto wake mdogo (Hassan) kisha kuanza harakati za kumsaidia mama yake na mtoto wake mkubwa (Zuhura) lakini hakufanikiwa kutokana na moto kuwa mkubwa.
“Hivyo mimi niliungua kichwani, mama yangu na mwanangu Zuhura miili yao ikaungua vibaya,” anasimulia.
Anaeleza kuwa baada ya moto kupungua, yule mganga na baba yake walikuja kuwasaidia kuwatoa ndani ya shimo huku wenzake wakiwa wameshaungua kiasi cha kushindwa kufanya lolote.
Baada ya kutolewa majeruhi hao baba yake na mganga walimshauri wasipeleke majeruhi hospitali wakawaeleza kuwa kuna daktari wao atakwenda kuwatibu katika kijiji cha jirani na hapo walimhakikishia kuwa majeruhi hao watapona.
Hata hivyo, Aziza anasema kuwa kwa daktari huyo hakuna kilichofanyika kwa zaidi ya siku tatu na ilipofika Desemba mosi mama yake alifariki dunia hapo hapo kijijini huku hali ya mtoto wake ikizidi kuwa mbaya kutokana na kukosa tiba.
“Kwa huyo mganga hakuna tiba waliyopata zaidi ya kubandikwa pamba kwenye vidonda vyao kwa siku zote tatu. Mama alifariki dunia kutokana na majeraha yake kuendelea kila siku na maumivu makali,” anasema Aziza.
Anasema kwamba jambo baya lililokuwa likiendelea kwa daktari huyo ni vidonda vya majeruhi kuanza kuharibika na kutoa wadudu hali anayosema ilianza kumtisha zaidi na kuanza kukata tamaa ya kupona.
Hospitali
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Handeni, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni Mwanaidi Semboja anasema kuwa walimpokea mgonjwa huyo (Zuhura) akiwa katika hali mbaya huku vidonda vyake vikiwa havijapata tiba yoyote.
Anasema baada ya kumpokea walianza kumpa tiba za kitaalamu zaidi ikiwemo kumpunguzia maumivu yaliyotokana na kuungua sehemu kubwa ya mwili wake hivyo kushindwa kufanya lolote.
“Kwanza tulianza kumpatia dawa za kumpunguzia maumivu kwani aliletwa akiwa kwenye hali mbaya sana kutokana na kutofungwa vidonda. Kitaalamu ili kuzuia baridi, tulianza kufanya hivyo na baada ya siku kadhaa mgonjwa aliendelea vizuri,” anasema.
Muuguzi huyo anasema kuwa kitaalamu binti huyo ameungua asilimia 72 na kwamba mgonjwa kama huyo anatakiwa kuwa na uangalizi maalumu kwa muda wote.
Semboja anasema kuwa wanawashukuru wasamaria wema waliotoa taarifa polisi ambao walifika walipohifadhiwa majeruhi hao, kisha kuwachukua kuwapeleka hospitali, ambapo yeye Aziza anaendelea vizuri, huku Zuhura akiendelea kupata tiba na kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa, Bombo mjini Tanga.
Wananchi
Aziza Mkomwa mkazi wa wilayani Handeni anashauri akisema kuwa ni vyema wananchi wakamrudia Mungu kwa kumwamini na kufanya ibada misikitini au kanisani, badala ya kuendeleza imani potofu ikiwamo matambiko.
Anasema ni muhimu kila mtu asimamie kwenye imani yake ya kidini kwa kufuata yale ambayo vitabu vitakatifu vinamwongoza badala ya kwenda kinyume na maagizo ya Mungu hata kukutwa na matukio ya ajabu kama yaliyomkuta Aziza na familia yake.
Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraisser Kashai anathibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema kuwa mtuhumiwa amekamatwa na hatua zaidi kuchukuliwa.
captions
Aziza Hassani akimuuguza mtoto wake Zuhura Rajabu(17) aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, baada ya kuungua mwili mzima walipokuwa wakifanyiwa dawa kwa mganga wa kienyeji ambapo mama huyo alipata majeraha madogo kichwani. Picha na Rajabu Athumani.
Picha namba 2.
Zuhura Rajabu (17) akiwa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Handeni akiuguza majeraha ya moto baada ya kuungua alipokuwa akifanyiwa tambiko yeye na familia yake kwa mganga wa kienyeji wilayani humo. Picha na Rajabu Athumani.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa