Home » » Upekee wa Hifadhi ya Saadani usiotangazwa

Upekee wa Hifadhi ya Saadani usiotangazwa


Kila hifadhi ya taifa ina upekee wake. Na hicho hukifanya kuwa kivutio kwa watalii. Hifadhi ya Taifa ya Saadani ina vivutio vya kihistoria kama vile wanyama, mito na bahari. Nadhani ni hifadhi pekee inayoweka pamoja vivutio vyote.
Kihistoria Hifadhi ya Saadani inapakana au kuhifadhi miji ya kihistoria kama Saadani wenywe, Utondwe, Kipumbwi na Mkwaja, Pangani, Buyuni Ukuu na Buyuni Kitopeni ambayo ingawa sasa haijulikani tena.
Katika zama zake ilikaribisha wageni wa kimataifa, au kuwa miji ya kibiashara (ya maliasili na watumwa) na kuwakaribisha wakoloni na kujenga miji.
Saadani ulikuwa mji mkubwa sana wakati wa ukoloni


 wa Wajerumani na pia kaburi la yule mmishenari maarufu aliyekuja kueneza Ukristo, hasa Mombasa, Tanga na Kilindi, Johannes Rebmann liko hapo hadi leo.
Hadi leo Kipumbwi bado ni bandari muhimu ya majahazi inayounganisha Wazanzibari na Watanganyika kwa kufanya safari kati ya kijiji hicho cha pwani na bandari kuu ya awali – Mkokotoni. Safari hizo ziko kila siku.
Miji ya Pangani, Bagamoyo na kijiji kilichopotea cha Utondwe vina mpatia fursa mtalii kuvifikia wakati anapotembelea hifadhi hiyo.
Utondwe unaandikwa na Wareno kama mji wa mashamba ya chumvi na askari wa Kizaramo wapiga mishale wazuri. Ushahidi ni msikiti wa kale uliopo hadi sasa huko Kitame, ingawa hautumiki.
Saadani ni hifadhi inayopakana na mito mitatu. Ruvu uko mbali lakini kuna Pangani na Wami. Mito hii mitatu kwa pamoja hukutana huko baharini na kutengeneza mkondo hatari wa Nungwi unaoleta vurugu katika majira fulani fulani.
Serikali ya Zanzibar kama ingekuwa na uwezo wa kifedha ungeweza kutengeneza bomba la kuvuta maji baridi kutoka kwenye kine kirefu cha Nungwi, yanayotokana na Ruvu, Wami na Pangani, mito mitatu inayopangana na hifadhi ya Saadani.
Pia, ndani ya mito hiyo unajifunza maisha na uhifadhi unaofanyika wa maisha ya majini na baharini ya wanyama na mimea.
Wakati ukiwa Mto Wami unajifunza maisha ya baharini na wanyama wake, Mto Pangani una hifadhi kubwa ya mapito ya kihistoria na biashara- utumwa, katani, mali ya asili, hasa meno ya tembo na nazi mbichi na mbata.
Ukisafiri katika Mto Pangani hadi huko ndani nchi kavu unakutana na vituo vya kihistoria ikiwamo mahali Bushiri bin Salim alipoishi, Matakani na Kijiji cha Bushiri.
- Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa