Home » » MSISHANGAE, CCM IMEGEUKA KUWA MNARA WA BABELI!

MSISHANGAE, CCM IMEGEUKA KUWA MNARA WA BABELI!

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Sasa ni dhahiri kwamba mwelekeo wa nchi yetu umetufikisha mahali pabaya. Haya tumeyasema, tumeyaandika, wengine tumeyahubiri, lakini serikali yetu tukufu ya CCM haisikiii.
Mara nyingi kwa watu waliosema hayo, wameonekana ni ‘maadui nambari wani.’ Ni kitu cha kusikitisha kwa taifa kama hili ambalo ni changa lakini lenye kubarikiwa na Mwenyezi Mungu.
Waswahili husema, penye miti hakuna wajenzi.’ Siasa za nchi yetu zilianza vyema na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye anaweza kufananishwa kama ‘Musa’ aliyewatoa Waisraeli utumwani.
Kazi ya kuleta ukombozi ni kazi ngumu kwa kiongozi na wanaowangoza, kwani inahitaji ubunifu, upendo, uzalendo, heshima, utu na uvumilifu mkubwa.
Mwalimu Nyerere alijenga taifa lenye umoja, heshima, undugu, usawa, upendo, amani na haki, chini ya siasa za ‘Ujamaa na Kujitegemea’ kama dira yake ikaimarishwa na Azimio la Arusha la 1967.
Mwalimu alijitahidi kufuta utemi na kuwaunganisha Watanzania wakazungumzia lugha moja ya kindugu. Hata hivyo, baada ya Mwalimu Nyerere kufariki dunia, viongozi waliofuata walianza kuachana na misingi mizuri aliyoiasisi. Leo, nchi yetu imegawanyika vipande chini ya Serikali ya CCM. Chini ya Mwalimu Nyerere, CCM ailikuwa na umoja, dira, sera nzuri, ilikuwa na upendo.
Ile ya Nyerere ilipendeza, kupendwa na Watanzania karibu wote. Lakini, CCM ya leo inayounda Serikali ya Tanzania imegeuka na kuwa kama ‘mnara wa Babeli’ (Mwanzo 11:19). Kwa nini naifananisha CCM ya leo na mnara huo maarufu? Ni kwa sababu ya hali halisi ya siasa katika nchi yetu. Waisraeli walipofika katika nchi ya Shinar walifyatua matofali na kujijengea mji na mnara ili kuichungulia mbingu kwa majivuno ya kujiona wao sasa ni sawa na Mungu.
Kisha, wakasema ngoja tujitengenezee jina kwa ajili yetu. Lakini, Mungu aliposhuka kutoka mbinguni alipoona jinsi walivyojaa majivuno, kiburi, dharau, ulevi wa madaraka akawasambaratisha kwa kuwachanganya wasisikilizane tena. ( Mwanzo 11:1-9). Na huo ndiyo ukawa mwisho wao.
CCM ya sasa imekuwa kama mnara wa Babeli, hakuna umoja, upendo, amani, kuamini, heshima, dira, sera za kujali wanyonge, kuwatumikia wananchi.
Ndani yake, kuna kejeli, vitisho, kiburi na ubabe. Kwa nini tuifananishe na Mnara wa Babeli? Askofu Mkuu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship alishatoa utabiri kama huo huo, kwamba CCM itasambaratika, na je, nini kinaendelea kutokea hadi leo hii na hasa ukitazama kinachojiri kwenye Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma? CCM inazidi kujikaanga kwa kupanga kila aina ya mizengwe, hila, fitina, unyanyasaji kwa raia na wapinzani kwa kutumia vyombo vyake.
Je, hii si alama ya kusambaratisha kama mnara wa Babeli? Mungu wetu ni Mungu wa haki, mtu mwenye fitina na chuki, hatafika mbali, maandiko yanasema.
Kuendelea kujidanganya kwamba CCM inapendwa na inakubaliwa na Watanzania wengi ni kuonyesha upofu wa hali ya juu, ulevi wa madaraka. Matokeo yake ni kulazimisha, kitu ambacho ni alama wazi ya kushindwa kuendesha nchi kwa kufuata sheria, kanuni na katiba
Bahati mbaya kuna wana- CCM na viongozi wa serikali ambao kwa makosa ya fikra, kiburi na utamu wa madaraka bado wanajidanganya na kuamini kuwa chama chao kitadumu milele. Hawa pamoja na mashabiki wao wapenda madaraka na mafisadi wamejiaminisha katika upotofu wao kuwa chama hiki kitatawala milele, kitadumu milele na kitaendelea kuwa kama kilivyo sasa milele na milele!
Hawa ni wale wanaotakiwa kuombewa kwani wana ‘pepo la ulevi wa madaraka’ ambao ni ugonjwa mbaya.
Niseme tu kwamba CCM ni tunda la fikra na kazi ya binadamu; ni chombo kilichoundwa na wanadamu, kinaongozwa na binadamu.
Kwa hiyo, CCM ni chombo kinachoweza kuharibika, kuvunjika, na mwishowe kinaweza kufa. Vyama vingi vikongwe Afrika kama vile, Kenya (KANU), Malawi (MCP), Zambia (UNIP) na kadhalika vilikufa.
Busara za kibinadamu zinatuambia,‘ kila kitu kina mwanzo na mwisho’. Hivyo, CCM lazima itafika mwisho kama siyo leo ni kesho, na kama siyo kesho, keshokutwa, hii ni kawaida.
Watu wengine wanapokaribia kufa huhangaika na kutapatapa wakijaribu kujiuliza kwa nini mimi, hutafuta mchawi wao ni nani?
Leo, CCM inahangaika kutafuta mchawi wake ni nani na inapoteza muda mwingi kushughulika na wapinzani, kuwadhibiti badala ya kujenga sera za kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la umaskini. Mchawi wa CCM ni wao wenyewe lazima ifike mahali wajitafiti. Nchi inadai mabadiliko, je wapo tayari kuyaongoza mabadiliko hayo kwa usalama na umakini?
Saikolojia ya magonjwa ya akili inatufundisha kwamba dawa pekee ya kupona magonjwa hayo kama ulevi wa dawa na pombe ni kujikubali kwamba una tatizo, la sivyo utaendelea kusteseka.
Hivyo, ninaposikia mtu anasema kwamba hakuna ufisadi ndani ya CCM anashangaza. Nikimsikia anayesema ‘CCM ni safi’, naendelea kumshangaa zaidi, nikisema mwenzetu anazungumzia CCM gani ya Mwalimu Nyerere au hii ya leo? Pia, ninapowasikia wapiga propaganda wa CCM wamekazana kuitetea kuwa ni chama safi na kina ‘mafisadi wanne’, ninafumba macho yangu na kujiuliza ‘hivi ni kweli’ au ni porojo?
Au hii ni alama ya kukata tamaa na alama wazi ya kugeuka mnara wa Babeli na ulevi wa madaraka. Matukio ya ajabu tunayoyasikia sasa na kuyashuhudia hivi sasa ndani ya CCM ni alama wazi kwamba chama hiki kikongwe barani Afrika hakika CCM iko matatani na hakuna mtu wa kuiokoa. Haiokoleki kwa sababu imegeuka na kuwa kama mnara wa Babel
 Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa