Home » » DC MUHEZA AAHIDI KUSIMAMIA UPIMAJI ARDHI WANANCHI WAPATE MAENEO

DC MUHEZA AAHIDI KUSIMAMIA UPIMAJI ARDHI WANANCHI WAPATE MAENEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Subila Mgalu
 
Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Subila Mgalu, ameahidi kusimamia upimaji ardhi wa shamba la mkonge Kibaranga ili wananchi wapate ardhi ya kulima.
 
Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika Kibaranga, baada ya kutokea mgogoro kati ya wananchi na maafisa ardhi waliyopewa kazi ya kupima shamba hilo.
 
Alisema kuwa kazi ya kupima shamba hilo imeanza lakini kuna baadhi ya watu wanaendeleza mgogoro kati ya wananchi na serikali.
 
Hatua hiyo inafuatia maafisa ardhi wilaya ya Muheza kuanza kupima shamba hilo ili wananchi wapatiwe maeneo ya kilimo.
 
Alisema kuwa baadhi ya watu  wanadanganya wananchi hao kuwa tayari maafisa ardhi wanagawa mashamba kwa kupewa kitu kidogo, kitu ambacho si cha kweli.  Alisema amesikitishwa na kitendo cha  wananchi hao kufukuza maafisa ardhi kwa kutumia mapanga wakati mchakato huo ukiwa unaendelea vizuri baada ya agizo la Rais Jakaya Kikwete la kukubali shamba hilo wapewe wananchi.
 
Alisema kuwa kwa sasa wanafanyakazi hiyo ya upimaji kwa shida kwani inatakiwa zaidi ya Sh. Milioni 100 lakini wanapima kwa Shilingi Milioni nane tu ambazo wamepewa na wafadhili kufanya kazi hiyo.
 
Mgalu alisema kuwa yupo tayari kufa ili kuhakikisha shamba hilo linapimwa ili wananchi wapewe ardhi hiyo.
 
Aliwataka wananchi kuwa wavumilivu ili zoezi hilo liende vizuri ili wananchi wapate ardhi.
 
Kwa upande wake Afisa ardhi ambae alikuwa anaendesha zoezi la upimaji shamba hilo, Daniel Mkwizu, alisema kuwa zoezi lilikuwa linaendelea vizuri lakini wananchi waliwafukuza  na mapanga na kulisitisha.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa