Home » » BAADHI YA WANAFUNZI KUZUILIWA MATOKEO KIDATO CHA PILI KOROGWE.

BAADHI YA WANAFUNZI KUZUILIWA MATOKEO KIDATO CHA PILI KOROGWE.


Na Thehabari.com, Korogwe

BAADHI ya Wanafunzi waliofanya mitihani wa mchujo wa kidato cha pili kuingia kidato cha tatu Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe huenda wakazuiliwa kupewa matokeo yao kutokana na kutokuwa na fomu namba 9 (TSM9) za uzajili katika shule zao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wilayani Korogwe, na kuthibitishwa na Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wilaya hiyo, miongoni mwa wanafunzi ambao wataathirika na tatizo hilo ni kutoka katika shule za sekondari Bungu, Patema pamoja na Mfundia.

Taarifa zinaeleza wanafunzi hao waliofanya mitihani yao ya mchujo ya kidato cha bila mapema kuanzia Novemba 5, 2012 bila ya kuwa na TSM9 namba, hivyo walimu wakuu wa shule husika kuamriwa wawasilishe namba za wanafunzi hao katika kituo cha kusaishia mitihani hiyo.

Akizungumzia tatizo hilo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Shaban Shemzighwa alikiri kuwepo kwa tatozo hilo na kudai walipokea malalamiko toka ya baadhi ya wanafunzi wa kidato cha pili juu ya utata wa suala la TSM9.
Hata hivyo alisema wanafunzi waliokuwa na utata juu ya suala la TSM9 waliruhusiwa kufanya mitihani yao ya mchujo na baadaye walimu  wakuu wa shule zao kuelekezwa wanatakiwa kuwasilisha namba za wanafunzi hao kwenye vituo vya kusahihishia mitihani ili waweze kutambulika.

“Taarifa za malalamiko zilitufikia na baadhi ya Shule za Sekondari ambazo wanafunzi walikuwa na matatizo hayo ni Bungu, Patema, Mfundia na nyinginezo, hapa nipo nje ya kituo cha kazi hivyo ni vigumu kutaja idadi na shule zote,” alisema Shemzighwa akizungumzia suala hilo.

Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na baadhi ya wakuu wa shule ambao shule zao limetajwa kuwa na tatizo hilo walikwepa kuzungumzia, huku wakidai hawakuwa na tatizo hilo kwa wanafunzi wao.

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli akizungumza na mwandishi wa habari hizi alipinga shule yake kuwa na tatizo hilo licha ya Kaimu Ofisa Elimu Sekondari kuitaja shule hiyo pia kukumbwa na tatizo la TSM9 kwa wanafunzi wake kwenye mitihani ya kidato cha pili iliyofanyika Novemba, 2012.
Jumla ya wanafunzi wa kidato cha pili 442,925 walifanya mitihani ya mchujo wa kidato hicho mapema Novemba 5, 2012 na watakaoshindwa kupata wastani wa alama 30 watachujwa na kulazimika kurudia kidato hicho kwa mwaka unaofuata.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa